Bukoba: Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera kimewafukuza uanachama
wa chama hicho, madiwani wake wanane kutokana na kile kilichoelezwa kuwa
ni kukaidi maelekezo mbalimbali ya chama hicho, pia kushirikiana na
upinzani kukihujumu.
Madiwani waliotimuliwa ni wale Manispaa ya Bukoba ambao wamekuwa
wakitajwa kumuunga mkono Mbunge wa Bukoba Mjini ambaye pia ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye amekuwa akivutana
vikali na Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Amani.
Miongoni mwa waliotimuliwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba na
Diwani wa Kashai, Yusuph Ngaiza, aliyepata kuwa mbunge wa muda mrefu wa
Bukoba Mjini na baadaye Meya wa Manispaa hiyo, Samuel Ruhangisa ambaye
ni Diwani wa Kitendagulo na Diwani wa Buhembe, Alexander Ngalinda ambaye
pia alikuwa Naibu Meya.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Averin Mushi alisema uamuzi wa
kuwatimua madiwani hao umefikiwa jana na halmashauri ya CCM ya Mkoa kwa
kile alichosema ni kwa ajili ya “kulinda masilahi ya chama na wananchi
wa Bukoba”.
Ibara ya 93 (15) ya Katiba ya CCM inataja moja ya kazi za halmashauri ya
chama hicho ngazi ya mkoa kuwa ni: “Kumwachisha au kumfukuza uongozi
kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri ya
CCM ya Mkoa”.
Hata hivyo kipengele cha 14 cha ibara hiyo ya 93 kinasema hatua
kumwachisha au kumfukuza mtu uanachama itachukuliwa endapo halmashauri
itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za
uanachama.
Hatua ya kuwafukuza uanachama madiwani hao ambao pia watakuwa wamepoteza
nafasi zao za udiwani, imekuja siku chache tangu Mwenyekiti wa CCM,
Rais Jakaya Kikwete alipozitaka pande zinazohusika katika mgogoro huo
kumaliza kwa njia ya mazungumzo.
“Madiwani wote wa CCM walioendelea na mgomo hata baada ya maelekezo ya
Mheshimiwa Rais kwa kusaini barua ya kutaka Mkurugenzi aitishe kikao cha
kumwondoa Meya tumefikia uamuzi mgumu wa kuwafukuza uanachama kwa
masilahi ya chama na wananchi wa Bukoba,’’ alisema Mushi.
Mushi aliwataja madiwani wengine waliofukuzwa ni Robert Katunzi
(Hamugembe), Deus Mutakyahwa (Nyanga), Richard Gasper (Miembeni),
Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu) na Dauda Kalumuna aliyekuwa Diwani wa
Ijuganyondo.
Katibu huyo alisema Balozi Kagasheki na Meya Amani ambao mamlaka yao ya
uteuzi ni ya kitaifa na wanatakiwa kumaliza tofauti zao kama
walivyoelekezwa na Rais.
Mgogoro uliosababisha madiwani hao kutimuliwa uliibuka baada ya
Kagasheki kumtuhumu Meya Amani kwamba ameingiza Manispaa katika miradi
ya ufisadi hali ilioibua makundi na kukwamisha kufanyika hata vikao vya
Baraza la Madiwani.
SOURCE:Chanel ten BUKOBA
No comments:
Post a Comment