ASKARI
mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoani Kilimanjaro, Fidelis
Mwaliyatabu, amefariki dunia papo hapo na wengine tisa akiwamo Mkuu wa
Kikosi hicho kujeruhiwa vibaya baada ya gari lao kupinduka katika
kijiji cha Kilingi, wilaya ya Siha, wakati wakienda kuzima vurugu za
wananchi.
Ajali
hiyo ilitokea wakati kikosi hicho kikielekea katika kijiji cha Karansi
kwa ajili ya kukabiliana na wananchi waliokuwa wakiandamana kupinga
wenzao waliokamatwa usiku wa manane baada ya kuvamia mashamba mali ya
Shirika la Roho Mtakatifu-Kilasara.
Taarifa
kutoka kijijini humo zilieleza kwamba wanakijiji waliamua kuandamana
baada ya wenzao watano kukamatwa na Jeshi la Polisi nyakati za usiku
kwa mahojiano kutokana na kukabiliwa na tuhuma za kushawishi wanakijiji
wenzao kuvamia maeneo ya Shule ya Kilasara na kusababisha hasara kubwa
kwa shule hiyo.
Kufuatia
kukamatwa kwa watuhumiwa hao, wanakijiji waliamua kuaandamana hadi
katika kituo cha polisi ili kuwatoa wenzao hali ilisababisha jeshi hilo
kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya, jambo ambalo lilishindikana
kutokana na wingi wa watu walikuwa wanaandamana.
Inadaiwa
kuwa wananchi hao walijikusanya na walianza kuandamana kuanzia majira
ya saa 7 usiku kuelekea kituo cha polisi ili kuwatoa wenzao walikuwa
wanashikiliwa.
Wananchi
wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni John Sokoine, Abeli Solomoni,
Christopher Solomon na aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Julius. Wote
walikamatwa usiku wa kuamkia jana.
Mnamo
Juni 11, mwaka huu majira ya mchana wananchi wa kijiji hicho walivamia
eneo lenye ukubwa wa hekta mbili na kufyeka mazao mbalimbali yaliyokuwa
shambani hapo kwa madai kuwa wamiliki wa shule hiyo wamechukua eneo
hilo kinyume cha taratibu.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu, Kanda ya Afrika, Padri
Jerome Okama, aliushutumu uongozi wa kijiji hicho kwa kuvifumbia macho
vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi wakati wakitambua kuwa
eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 8.9 linamilikiwa na shirika hilo
kihalali.
Kamanda
wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya
simu kutoka wilayani humo jana jioni, alisema askari hao walipata ajali
hiyo majira ya saa 6.45 mchana katika kijiji cha Kilingi nje kidogo ya
mji wa Sanya Juu.
Alisema
askari hao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na wengine
wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu ya
Kibong'oto ilioyopo wilayani Siha na kwamba watano kati yao hali zao ni
mbaya.
Alitaja
gari la Polisi lililopinduka na kuua kuwa ni Toyota Land Cruiser lenye
namba PT 2070 lililokuwa likiendeshwa na Sajenti Herman Dancan. Chanzo
cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kuacha njia na kupinduka.
Aliwataja
waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Mkuu wa FFU mkoani hapa, ASP
Nonino, Renatus Misigalo, Alfonce Joseph, Koplo Elifuraha Lenare, Peter
Albert, Bashiri Yusuph, George Mwakyusa na Gaspar Mwapunda.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Kibong'oto.