WANAJESHI
saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa
wakati wakilinda amani Darfur nchini Sudan, walipigana kwa saa mbili
wakati wakijitetea kabla ya kufikwa na mauti.
Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema hayo
jana Dar es Salaam, wakati akitoa salamu za rambirambi, wakati wa kuaga
askari hao waliouawa Julai 13.
Katika
shughuli hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ),
Rais Jakaya Kikwete aliongoza waombolezaji kuaga mashujaa hao ambapo
pia Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na mawaziri mbalimbali
walihudhuria.
“Kikundi
hicho (askari wa JWTZ) kilikuwa kikitokea eneo la Abeche, kwenda Nation
na kilipofika umbali wa kilometa 25, doria hiyo ilipunguza mwendo
kutokana na utelezi wa matope yaliyosababishwa na mvua.
“Ghafla
kikundi hicho kilishambuliwa na watu ambao hawakufahamika, wakitumia
silaha nzito za kivita,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema
ulikuwa ni mtego wa mashambulizi na kwa mujibu wa taratibu za
operesheni hizo, doria hiyo haikuwa na silaha nzito, lakini ililazimika
kujibu mapigano hayo hadi kikundi kingine cha askari wa JWTZ,
kilipoitwa kuongeza nguvu kunasua wenzao katika mtego huo.
Jenerali
Mwamunyange alisema wakati kikundi hicho kikinasuliwa, askari hao
walipoteza maisha kwa ujasiri mkubwa na wengine 14 kujeruhiwa.
Alisema
Tanzania imefikwa na msiba huo wa mashujaa, ikiwa imeshiriki kulinda
amani Sudan tangu mwaka 2007, ambapo askari wake wamekuwa wakitekeleza
majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu, kwa kushirikiana na vikundi
vingine na wenyeji katika maeneo ya operesheni.
Majina
yao Awali Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alitaja majina ya
mashujaa hao na mahali wanapokwenda kuzikwa, kuwa ni pamoja na Sajini
Shaibu Othman (Zanzibar) na Koplo Osward Chaulo (Kilolo, Iringa).
Wengine ni Koplo Mohammed Ally (Zanzibar), Koplo Mohammed Chukulizo
(Kigoma), Praiveti Rodney Ndunguru (Songea), Praiveti Fortunatus Msofe
(Tanga) na Praiveti Peter Werema (Tarime, Mara).
Rais
Kikwete alisema mauaji ya wanajeshi hao, yalimshitua, kumhuzunisha na
kumkasirisha na kujikuta akijihoji kwa nini watu wa Sudan waue
Watanzania.
Alisema
Watanzania hao walikwenda kuwasaidia kupata amani, utulivu, kunusuru
maisha yao na kuwaondolea mazingira ya wasiwasi ili wafanye shughuli
zao kwa tija.
Alisema
tangu kuanza kwa shughuli za ulinzi wa amani Darfur, walinzi wa amani
41 kutoka mataifa mbalimbali wameuawa, na 55 kujeruhiwa na hakusita
kuamini kuwa waliofanya tukio hilo ni wasiotaka amani Darfur.
“Idadi
hii ni kubwa, inahitaji kutafakari vizuri na kutazama upya mfumo wa
kiwango cha kujilinda kwa wanajeshi… lazima uwezo huo uongezwe ili
kupunguza vifo zaidi,” alisema Rais Kikwete.
Aliahidi
kufikisha maombi hayo kwa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa
(UN), ili walitazame vizuri. Mchango wa Tanzania Rais Kikwete alisema
Tanzania tangu Uhuru imekuwa ikijitolea kusaidia wanyonge dhidi
ubaguzi, uonevu na wengine ambao njia za diplomasia zimekuwa zikitumika.
Aidha,
alisema wakati wote walipoombwa, walijua uwezekano wa askari wao
kujeruhiwa au kupoteza maisha, ni mambo yaliyofikiriwa kuwa yanaweza
kutokea kwani walikwenda kwenye maeneo ya hatari, yenye mapigano.
Alisema
kutokea hayo si ajabu, lakini hadhari kubwa ilichukuliwa kwa kupewa
mafunzo, zana za kujihami, kujilinda na kutekeleza majukumu.
Rais
Kikwete alisema baada ya mauaji hayo ya Darfur alizungumza na Katibu
Mkuu wa UN, Ban Ki-moon ambaye alielezea masikitiko yake na kutoa pole
nyingi, na kueleza kwamba alizungumza na Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir,
ili achukue hatua ya kusaka na kuwaadabisha wahalifu hao.
“Nami
pia nilifanya mazungumzo na Rais wa Sudan, na alielezea masikitiko yake
na nilimsisitizia umuhimu wa Serikali yake kufanya hivyo, kwa kuwa
tukio hilo limetokea huko na hivyo waliofanya hivyo ni Wasudani,”
alisema Rais Kikwete.
Alisema
alimsisitiza, kwamba kwa kuwa mauaji hayo yamefanyika katika mamlaka ya
Sudan, waliohusika wawe Waasia au Wasudani, lakini achukue hadhari zote
kuwasaka.
Waziri
Ulinzi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha,
alisema Watanzania wamesikitishwa na mauaji hayo na inaweza kuwa
mkakati wa kufifisha juhudi za UN kuleta amani.
“Wizara itatoa kila msaada kuwezesha maziko na kusaidia familia za marehemu na waliojeruhiwa,” alisema Nahodha.
Akitoa
salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed
Shein, Meja Jenerali Salum Mustapha Kijuu, Kamanda wa Kikosi cha Nchi
Kavu, alisema tukio hilo linasikitisha na ni msiba wa Taifa kwa kuwa
askari hao walikufa kazini na ni mashujaa.
Katika
eneo hilo, miili ya wanajeshi hao iliingia kila mmoja kwa gari maalumu
la Jeshi na kupokewa na maofisa wa JWTZ na kupelekwa sehemu
iliyoandaliwa kuagwa. UN itatoa medali kwa kila askari, kwa kutambua
mchango wao.
No comments:
Post a Comment