BAADHI
ya wagonjwa wa Saratani waliolazwa katika Taasisi ya Saratani Ocean
Road mjini Dar es Salaam, wamebainika wanatumia mafuta ya ubuyu wakati
yanadaiwa kusababisha saratani ya ini. Uchunguzi uliofanywa na
MTANZANIA katika taasisi hiyo, umebaini wagonjwa wengi wanatumia mafuta
hayo kwa usiri mkubwa. Katika hatua nyingine, Chama cha Albino Tanzania
(TAS), kimewataka watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), wanaotumia
mafuta hayo kuacha mara moja, hadi hapo Serikali itakapotoa taarifa
rasmi kuhusu matumizi ya mafuta hayo kwa ngozi ya albino.
Katika
uchunguzi huo, imebainika baadhi ya albino hutumia mafuta hayo kwa
kujipaka huku wengine wakiwa na vidonda kwenye ngozi zao.
Akizungumza
na MTANZANIA, Katibu wa Chama hicho Taifa, Ziyada Nsembo alisema, TAS
hakina elimu kuhusu bidhaa hiyo, hivyo wanaotumia wanaweza kuathiri
ngozi zao zaidi.
“Tunawataka
albino wanaotumia mafuta haya waache mpaka Serikali itakapotoa tamko
rasmi kuwa mafuta hayo hayana athari kwa ngozi ya albino.
“Ngozi
ya albino ni nyepesi, ina uwezo mkubwa wa kupitisha kemikali ndani ya
mwili, ikiwa hayafai kunywa basi kwetu hayafai hata kujipaka, maana
wengine wana vidonda.
“Tumeamua
kutoa kauli hii kwa sababu kuna mafuta ambayo albino hatakiwi kupaka
mchana, huwa hayana uwezo wa kukinga mionzi ya jua.
“Haya
mafuta ya ubuyu tunaelezwa kuwa yanalainisha ngozi, hatujui kama
yanakinga ya mionzi ya jua, hilo ndilo tatizo letu, tunashauri
yasitumike hadi wataalamu wa masuala ya ngozi ya albino watufahamishe,” alisema Katibu huyo.
Mmoja wa albino ambaye ni kiongozi, alisema ameshawahi kutumia mafuta hayo.
“Wapo albino wanaotumia haya mafuta, hata mimi ni mmoja wapo, ila sikujua kama yana madhara, kwa sasa nimeacha kutumia.”
No comments:
Post a Comment